Mtagusano wa Kifonolojia baina ya Kinyankore na Kiswahili: Mtazamo wa Uwililugha Darasani
Abraham Kubakurungi Kyangungu, Mosol Kandagor & Samuel Obuchi
Chuo Kikuu cha Moi, S. L. P. 3900-30100, Kesses, Eldoret, Kenya
Email; kubakurungiabraham@gmail.com
Ikisiri: Makala hii inachanganua athari ya Uwililugha na jinsi L1 ya Kinyankore inavyoathiriana na L2 ya Kiswahili katika kiwango cha kifonolojia wakati wa masomo darasani. Utafiti huu ulilenga kutathmini athari ya L1 iliyo Kinyankore kwa mafunzo ya L2 iliyokuwa Kiswahili kwa kiwango cha kifonolojia. Pili, kubainisha mbinu za kukabili athari za kimatamshi katika ujifunzaji wa Kiswahli. Utafiti huu ulifanywa katika taasisi za elimu zilizochaguliwa jijini Mbarara, nchini Uganda, na ulifanyika kwa wanafunzi pamoja na walimu, walimu wakuu na maofisa wa Elimu katika kipindi cha miezi mitatu. Ili kufanya utafiti huu, nadharia mseto kama vile nadharia ya uchanganuzi Linganishi (Contrastive Analysis) na uchanganuzi wa makosa (Error Analysis) zilizingatiwa. Matokeo katika utafiti huu yanapendekeza kuwa uchanganuzi Linganishi CA na uchanganuzi wa makosa EA ni njia mwafaka za kusoma na kuelewa jinsi lugha ya kwanza (L1) ya mwanafunzi inaweza kuwa na ushawishi katika mchakato wa kujifunza lugha ya pili. Kulingana na utafiti, wanafunzi wengi waliathirika na sarufi ya kinyankore katika ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya pili. Iligunduliwa kwamba mtagusano huo ulitokana na athari za lugha yao ya kwanza.
